MJADALA mkali uliibuka bungeni jana baada ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema) kuwalipua baadhi ya viongozi waandamizi wa Serikali akitaka wachunguzwe kwa makosa ya kuficha mabilioni ya fedha nje ya nchi
Zitto alitoa kauli hiyo 
jana bungeni wakati akiwasilisha hoja yake binafsi kuhusu kulitaka Bunge 
kuchunguza na kuielekeza Serikali kuchukua hatua dhidi ya raia wa Tanzania 
walioficha fedha na mali haramu nje ya nchi.
Bila ya kuwataja kwa 
majina, mbunge huyo aliwataja watu hao kwa nyadhifa kuwa ni watu wote walioshika 
nyadhifa za uwaziri mkuu katika kipindi cha 2003 hadi 2010, walioshika nyadhifa 
za uwaziri wa nishati na madini katika kipindi hicho na waliokuwa makatibu wakuu 
Wizara ya Nishati na Madini.
Wengine ni mawaziri na makatibu wakuu wa Wizara ya 
Ulinzi, wakuu wa majeshi, wanasheria wa Serikali, makamishna wa nishati, 
walioshika wadhifa wa Ukurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli 
Tanzania (TPDC), Uenyekiti na Ujumbe wa Bodi wa TPDC katika kipindi cha mwaka 
2003 hadi 2010.
Kutokana na hilo, Zitto aliitaka Serikali kupeleka 
bungeni muswada wa sheria bungeni wakati wa Mkutano wa 11 wa Bunge wa Aprili 
mwakani.
“Mbali na hilo napendekeza kuwa iwe ni marufuku kwa 
kiongozi yeyote wa umma au mume au mke wake au mtoto wake kuwa na akaunti nje ya 
nchi isipokuwa kwa sababu maalumu na kwa kibali rasmi kutoka kwa Rais wa Jamhuri 
ya Muungano,” alisema Zitto
Pia Zitto alitaka Serikali kuwasiliana na Benki ya 
Dunia kupitia kitengo cha ‘Assets Recovery Unit’ ili mabilioni ya fedha na mali 
ambazo zimetoroshwa nje ya nchi kwenda Uswisi, Dubai, Mauritus na maeneo mengine 
ziweze kurejeshwa.
Aliwataka Watanzania wote wenye akaunti za fedha nje 
ya nchi waeleze wamezipata wapi na Takukuru wachukue hatua za kisheria dhidi ya 
watu wote wanaomiliki fedha hizo kinyume cha sheria.

No comments:
Post a Comment